Utangulizi
Mkwawa alikuwa Chifu (Mtwa) wa Wahehe ambaye alipata umaarufu mkubwa kwa kuwashinda Wajerumani pale Lugalo tarehe 17/8/1891 na kuendelea kuwapinga kwa miaka saba mpaka alipojiua mwenyewe kwa risasi. Jina la Mkwawa linatokana na jina la Mukwava kifupi cha Mukwavinyika, ikimaanisha mshindi wa nchi nyingi. Alizaliwa Luhota mwaka 1855. Uhehe iko mkoa wa Iringa kusini magharibi mwa Tanzania, Afrika Mashariki, Wahehe wanazungumza Kibantu. Historia ya Mtwa Mkwawa muda wote ilikuwa inanivutia tangu nilipokuwa mtoto mdogo. Baaada ya kupata elimu ya kutosha ya teknolojia ya habari, wazo la kuandika historia yake kwenye mtandao lilikuwa likigonga mawazo yangu. Kikwazo kikubwa kilikuwa ni maendeleo ya teknolojia ya habari, ilikuwa nyuma. Baada ya kupata mwanga ya teknolojia ya habari, juhudi zangu zilipata uhai. Hatua ya kwanza kubwa niliyoifanya ni kufungua domain mkwawa.com. Hata hivyo kikwazo kikubwa bado kilikuwepo, sikuwa na chanzo cha habari za kuaminika kabla ya kuziandika kwenye mtandao. Kwa bahati nzuri, mtengenezaji wa filamu kutoka Ujerumani, Ndugu Martin Baer, aliingia kwenye tovuti yangu http://www.mkwawa.com/immkwawa wakati akitafuta kizazi cha Mtwa Mkwawa kwenye mtandao. Yeye pia alikuwa alikuwa anavutiwa na historia ya Mtwa Mkwawa na alikuwa na mpnago wa kutengeza filamu tokea mwaka 1996. Alifanikiwa kupata pesa za kufanya hivyo na akanichagua kuwa mwigizaji mkuu. Nilichukua nafasi hiyo kukusanya hadithi na habari za uhakika kuhusu historia ya Mtwa Mkwawa wakati tukipiga picha za filamu Tanzania na Ujerumani. Nashukuru sana kwa vyote nilivyokusanya toka kwa watu, kusoma vitabu na kutembelea sehemu za historia. Hii ni matokeo ya safari yangu. Namatumaini makubwa kuwa mtandao huu utakupa elimu kubwa na kukufurahisha. |